Thursday, May 24, 2012


Simanjiro waanza kukeketa watoto wachanga, Madaktari wasema madhara zaidi yataongezeka
Huyu ni ngariba aliyekeketa maelfu ya wasichana katika eneo hilo

Fredy Azzah

WAKATI serikali pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka ndani nan je ya nchi yakitafuta njia ya kupambana na ukeketaji, ndivyo jamii inayoabudu mila hizi potofu wanavyotafutwa njia ya kutekeleza ukatili huo bila kubainika.
Jamii ya wananchi wa Simanjiro ambayo asilimia 95 ya wakazi wake ni wamasai na waarusha, wamebadili kutoka kufanya ukeketaji kwa wasicha wenye umri mkubwa uliokuwa ukikadiriwa kuwa 14 mpaka 18 na sasa ni watoto  wadogo wenye wiki moja mpaka mwezi mmoja.

Nang’urutu Kariayi (49), mkazi wa Narokusoito kata ya Langai, ni ngariba maarufu katika eneo hilo ambaye alianza kazi yake hiyo zaidi ya miaka 10 iliyopita, anathibitisha hilo akisema kuwa lengo kuu ni kukwepa kukamatwa na kuweza kulinda mila za kabila hilo.

 “Kwa siku nakata hata zaidi ya 10 kwa sababu kwa mtu mmoja anaweza akawa ana mabinti watano, na ile kitu siyo ngumu kwa sababu haina mfupa,” anasema Kariaya baada ya kutaka kujua idadi ya watoto anaowakeke kwa mwaka.


Anasema wakati masika kwake huwa siyo huwa na furaha yakupata nvua ya kustawisha mazao yake tu, ila pia ni kipindi cha kupata fedha kwani wakati huu ndiyo  shughuli za tohara kwa waume  na ukeketaji kwa wasichana ambao watu wa eneo hili wanaujua kwa jina la Emurata Ndito, ndiyo hufanyika.

“Wakati wa masika ndiyo huwa nakeketa kwa sababu huwa kuna baridi na damu za watoto zimetulia, hakuna mtu anaangaika kutafuta majani kwa ng’ombe, kwa hiyo alifajiri tu nakeketa hata zaidi ya 10,” anasema mama huyo aliyekuwa akizungumza kwa msaada ya mkalumani kutokana nayeye kutoelewa vizuri kiswahili.

Anasema licha ya kuwa kwa wauname kutahiriwa hufanyika kwa msimu ili kupata marika mbalimbali, yaani tohara kufanywa kwa miaka saba mfululizo kasha kusitishwa kwa kipindi cha miaka saba kabla ya kuanza tena, kwa wanawake ukeketaji huwa hauna msimu.

“Kwa wanake hakuna msimu kwa kuwa watoto wanakua kila siku, lakini siku hizi huwa unafanyika kwa siri kwa sababu Serikali haitaki,” anasema mama huyo.

Anasema kuwa, hakuna mtu aliyemfundisha kufanya kazi hiyo lakini kwa kuwa yeye mwenyewe aliona jinsi alivyokeketwa kisha kumuona mama yake mzazi ambaye alikuwa ngariba pia akifanya kazi yake, nay yeye sasa ni fundi wa kufanya shughuli hiyo ambayo kwake ni kazi inayompa kipato cha kula na watoto wake 10 alioachiwa ma mumewe ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Mimi mwenyewe nimekata ya ndito (wasichana) yangu nne,” mama huyu ambaye muda wote alikuwa akizungumza msaada wa mkalumani alieleza maneno hayo mwenyewe huku akionyesha ishara kwa kidole pia.

Hata  hivyo ngariba huyu anasema kuwa, tofauti na zamani ambapo walikuwa wakikeketewa wasichana ambao walikuwa karibu na kuolewa, siku hizi wanaokeketwa ni wenye kati ya miaka sita na saba.

“Ukiacha wanakuwa wanapata akili wanakataa kukeketwa au wakati mwingine wakianza shule wanaingiziwa mambo ya ajabu yanayowafanya wakae mila zao,” anasema ngariba huyu.

Anasema kazi hiyo aliinza akiwa na watoto watano na kuwa, zamni walikuwa wakifanya kwa ujira wa kupewa mbuzi kwa kukeketa mtoto mmoja lakini siku hizi huwa kukeketa mtoto mmoja ni Sh20,000.

Kwa kujiamini mama huyu anakiri kuwa anajua sharia inakaza ukeketaji lakini anasema kuwa, anaamini hawezi kukamatwani kwani kukeketa ni mila ya kimasai na hakuna mmasai anayeweza kumsemea kwa vyombo vya dola mpaka akamatwe.

“Bado wamasai wanapenda mila zao, siyo rahisi watoke wakaseme kuwa kuna mtu anakeketa, ukweli hakuna masai asiyekeketa, hata hao wa mjini wapo ambao huwa wanarudisha watoto wao huku nakuja kuwa keketa,” anasema mama huyo.

Ngariba huyu anaenda mbali zaidi kusema kuwa, hata viongozi wa vijiji hawawezi kufanya lolote kwani, wenyewe pia wanampelekea watoto wao ili awakekete.

Ngariba huyu anasema, sababu kubwa inayofanya vitendo hivi kuendelea katika jamii ya kimasai, ni kulinda mila za kabila hilo.

Anasema pia kuwa, sababu nyingine ni za kiafya ambapo hukeketa watoto ama hata watu wazima wakiwa wanaumwa ugonjwa alioutaja kwa jina la lawalawa.

Anasema kuwa, hata kama mtu amesha keketwa akiumwa tena ugonjwa huu wa lawalwa, huchanjwa sehemu zake za siri haswa maeneo ambayo yameathirika sana kasha kuwekewa dawa za kienyeji.

“Hii dawa ni chungu, lakini tumekuwa tukiitumia muda wote na watu wanapona,” anasema.

Hata hivyoMganga Mkuu wa Hospitali ya Orkesment anasema ugonjwa huo wa lawalawa kitaalam unajulikana kwa jina la Urinary tract infection ama kama wengi walivyo zoea kuuita (UTI).

Dk Loishorua Ole Yamat anasema kuwa, anasema kuwa watoto wengi na hata baadhi ya watu wazima huugua ugonjwa huo kutokana na kukaa uchafu.

“Utakuta wanafunika watoto na nguo chafu, hawawafanyii usafi wa kutosha, sasa wakiuguwa huo ugonjwa wao wanawakeketa, lakini UTI ni ugonjwa ambo unatibika hospitali kiurahisi tu, ndani ya wiki moja unameza dawa unapona,” anasema Dk Ole Yamat.

Anasema kuwa, mara nyingi jamii ya eneo hili imekuwa ikishikilia imani hiyo kwa muda mrefu sasa huku akisena kuwa, hatua ambayo jamii hiyo imefikia ya kuwakeketa watoto wadogo inaongeza mazara ya kitendo hicho mara dufu.

“Ukimkeketa mtoto mdogo unaongeza hatari ya kumwambukiza maradhi mengine kwa kuwa bado kinga yake ipo chini siyo kama mtu mzima, lakini pia hata wakati wa kumkeketa anaweza kuumia sana kwa sababu ya kuangaika kutokana na maumivu atakayo sikia,” anasema Dk Ole Yamat.

Jacobo Lemburis mkazi wa Orkasmenti anasema kuwa, licha ya eleimu kusambazwa katika eneo hilo juu ya madhara ya ukeketaji  wananchi hao wamekuwa wagumu kuachana na vitendo hivyo.

Anasema licha yam zee aliyemtaja kwa jina la Ngatai Lepilali mkazi wa eneo hilo kukeketa mtoto na kupoteza maisha, bado wanajamii wa eneo hilo hawajapata funzo.

“Badala ya kuachana na hali hiyo sasa wanakeketa watoto wadogo,” anasema.

Lemburis naye anaungana na Ngariba Kariaya kwa kusema kuwa, ukeketaji hufanyika zaidi wakati wa masika huku yeye akitoa sababu ya kuwa na mifuho iliyonona kuwa ni moja ya sababu ya wakati huo kutumika zaidi kwa shughuli hiyo.

“Wakati wa masika utakuta mifugo imenona kwa hiyo waliokeketwa hawakosi chakula, na watu wanakuwa hawangaiki kwa shida ya maji wala chakula kwa mifugo,” ansema  Lemburis.

Anasema kuwa, sababu za kuwakeketa ni ili wasiwe Malaya, na pia wawe na busara.

“Kwa masai mwanamke ambaye hajakeketwa hata kama ana miaka mingapi, yeye anaonekana tu kuwa ni mtoto mdogo na hana busara yoyote,” anasema Lemburis.

Anasema kuwa, katika eneo hilo hawezi kusema kuwa vitendo hivyo vimepungua kwani ila ni kuwa stahili imebadilika kutoka kukeketwa kwa sherehe na kufanya siri.

Anaeleza pia kuwa, kukomeshw kabisa kwa hali hiyo kunakuwa kugumua kutokana na mangariba kufanya shughuli hiyo kama kazi yao ya kuwapatia kipato.

Naye Martha Okida ambaye ameshawahi kufanya shughuli za uhamasishaji ili watu waachane na tabia hiyo, anasema bado hali ni mbaya sa.a

“Tuliwahi kwenda katika shule mbalimbali za msingi, ukiwapa watoto karatasi waandaike kama wamekeketwa ama laa, kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu tu, unaweza kukuta watano tu ndio hawajakeketwa, na wanakwandikia mpaka majina ya mangariba walio wakeketa,” anasema Okida.

Mama huyu pia anasema kuwa, wanasiasa kwa kiasi kikubwa wanakuwa na kigugumizi kukemea vitendo hivyo kwa kugopa kupotea nyadhifa zao.



Naye Naishie Saitoti Mkazi wa Kijiji cha Langai anasema kuwa, kuacha mila hiyo ni vigumu huku akisema siyo wamasai pekee wanaokeketa.

“Kwani sisi tuache, mbona kuna makabila mengi tu wanakeketa, bibi zetu walikeketwa na mama zetu lakini walituzaa, kwanini sisi tusiwakekete watoto wetu,” anasema mama huyo.

Wati utafiti uliofanywa na Mwananchi  kwa ushirikiano na Tamwa ukibaini hayo,baadhi ya wanasiasa wakiwamo madiwani na wenyeviti wa vijiji, wanasema kwa kiasi kikubwa hali ya ukeketaji haipo kwenye maneo yao.

Diwani wa kata ya Orkasiment Naftal Samuel, anasema kuwa katika eneo lake hajawai kuona vitendo vya ukeketaji vikifanyika kwa muda mrefu sasa hali inayomfanya aamini kuwa vitendo hivyo vimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Zamani ilikuwa ni rahisi kujua kama kuna watoto wanakeketwa kwa sababu kulikuwa na sherehe kubwa tu zinafanyika watoto wakikeketwa lakini siku hizi hakuna hayo mambo,” anasema Samuel.

Naye Diwani wa Langai Jackson Lesikari anasema kuwa, kwa kiasi kikubwa vitendo hivyo ktika eneo lake havipo, na kuwa wananchi wamebadilika baada ya kupatiwa elimu juu ya madhara ya vitendo hivyo.

“Ukeketaji wameacha kabisa baada ya kipewa elimu, watu wanaotoa elimu wanashirikiana na malaigwanani (vaiongozi wa kimila wa kimasai),” anasema Lesikari

Anasema kuwa, shirika lisilokuwa la kiserikali la Nafgem, linalotoa elimu juu ya ukeketaji, kwa kiasi kikubwa limefanikiwa kupunguza tatizo hilo kwa wanajamii hao.

Mwenyekiti w Kijiji cha Lolumorijei Jeremia Lemandi, anasema kuwa katika eneo lake vitendo vya ukeketaji vimepungua huku akisema kuwa, kwa kiasi kikubwa wanawake ndiyo wanaojua ukweli wa vitendo hivyo kwani ndio huvitekeleza.

“Wakinamama ndiyo wanakeketa, ukiwauliza ndiyo watakwambia vizuri,’ Lemandi.

Ingawa Lemandi anasema hayo, watu mbalimbali wa eneo hili wanasema kuwa, mtoto ni mali ya baba na wala mama hana sauti yoyote juu yake na hivyo baba ndiye mwamuzi wa kila jambo kwa binti yake ikiwa ni pamoja na kuamua akeketwe aole na mambo mengine kam hayo.



Naye Naomi Meshilieki anasema kuwa, kwa kiasi kikubwa wanafunzi ambao wanaingia shuleni bila kukekeketwa, hufanyiwa vitendo hivyo wakati wa likizo ama wakati mwingine kusingia shuleni kuwa wanaumwa.

Mkuu wa Shule ye Simanjiro Jacobo Khahima  anasema kuwa, ni vigumu kuainisha madhara ya ukeketaji kwenye elimu kwa kuwa vitendo hivyo hufanyika kwa usiri mkubwa.

Lakini Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya hiyo  Jackson Mbise, anasema kwa kiasi kikubwa vitendo hivyo vinachangia katika kudidimiza elimu katika eneo hilo.

Anasema kuwa, sababu zinazochangia hali hiyo ni mafunzo ambayo mabinti hupewa wakati wa kukeketwa ambayo huwafanya kujiona kuwa ni watu wazima na wanaweza kufanya chochote.

“Wakitoka huku wanakuwa tayari wameondolewa kwenye mazingira ya kishule shule, wanajiona sasa wao ni watu wazima wapo tayari kutembea na wanaume na kujenga familia, elimu kwao huwa ni kitu kidogo sana,” anasema.

Anasema kuwa, hali hiyo ndiyo sasa husababisha mimba na wengine kuacha shule na kuolewa, mambo ambayo kwa ujumla wake anasema yanaporomosha elimu katika eneo hilo.

Mrakibu wa Polisi Wilaya ya Simanjiro (ASP) Felix Kikwala, anasema kwa kiasi kikubwa kuwakamata watu wanaotekeleza vitendo hivyo noi vigumu kwani vinafanyika kwa usiri wa hali ya juu.

Kwa upande wake Ofisa Mradi wa Shirika linalotoa Elimu Juu ya Madhara ya ukeketaji Nafgem, Michael Nyari, anasema kwa kiasi kikubwa wanetoa elimu katika jamii ya eneo hilo juu ya madhara ya vitendo hivyo.

Anasema moja ya changmoto wanayokabiliana nayo nikuwa, jamii ya kimasai inaheshimu sana vitendo vya ukeketaji hivyo wakati mwingine inauwa vigumu kuacha kabisa mila hizo.

“Wamasai ni watu wenye siri sana, wanatekeleza hivi vitendo sasa katika hali ya usiri na hata hao wanaofanyiwa kati ya mambo wanayofundishwa ni kuwa wasiri na kutunza mila zao, wanaamini wakizivunja wanaweza kulaaniwa hata wakapoteza maisha,” anasema Nyari.

Moja ya mambo yanayoelezwa kuwa yanaweza kukomesha vitendo hivyo ni pamoja na mangariba kupewa njia nyingine ya kuendesha maisha yao kwani wengi wamefanya shughuli hiyo kuwa ni mired.

Jambo linalothibitishwa na Ngariba Kariayi anayesema kuwa, shughuli ya ukeketaji ndiyo inayomuwezesha kutunza watoto 10 alioachiwa na marehemu mume wake.

“Sasa hivi kwanza mimi nimeshakuwa hata mkirsto, nikiweza kupata kitu kingine cha kufanya nitaachana hata hii kazi,” anasema ngaiba huyo.

Hata hivyo pia wanasiasa wanatakiwa kubadilika na kuwa na ujasiri wa kukemea vitendo hivyo badala ya kuwa na sura tofauti katika kutekeleza vita dhidi ya vitendo hivyo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halamashauri ya Wilaya hiyo Patrick Saduka, anasema kuwa kwa sasa wanafanya uchunguzi ili kujiridhisha kama kweli kuna vitendo vya ukeketaji kwa watoto.

“Tulikuwa na kikao hivi karibuni tukishauriana jinsi ya kujiridhisha na taarifa zilizopo, tulifikiri labda watoto wakija kiliniki wakaguliwe lakini tukaona kuna changamoto zake, kwa hiyo bado tunaumiza kichwa kuangalia jinsi ya kubaini hilo,” anasema Saduka.

Anasema pia kuwa, katika kupambana na suala hilo mmoja wa ofisa wa Halmashauri hiyo anashirikiana kwa ukaribu na shirika lisilo la kiserikali la Nafgem ili kupata maelezo ya kina juu ya ukubwa wa tatizo hilo.

No comments:

Post a Comment