Thursday, May 24, 2012

Wanawake wa kimasai wanavyotaabika baada ya waume zao kumaliza ngombe, maelfu wazitoroka nyumba zao 


UTELEKEZWAJI wa watoto na wanawake, unatofautiana kulingana na maeneo na mila za jamii ya eneo husika.Katika maeneo ya mijini na hata kwenye baadhi ya Vijiji, utelekezwaji huu huwa ni wa kuwarudisha wanawake nyumbani kwao ama kuwafukuza na kwenda wanapojua.Lakini katika maeneo ya Masaini na hususani Simanjiro, hali ni tofauti, utelekezwaji unafanyika kwa wanaume kuondoka majumbani kwao na kuwacha wanawake na wakiendesha familia mbazo ni kubwa ama kuendelea kusihi nao lakini shughuli zote za familia wakiachiwa wao.
Ana Moreta (49) mkazi wa Kijiji cha Narokusoito kata ya Langai, ni mwathirika wa ulelekezwaji huo, ambapo sasa ana mzigo wa kuendesha familia yenye watoto nane baada ya mume wake kuondoka nyumbani na kwenda kusikojulikana.Kutokana na kutokuwa na mashamba wala mifugo, kwa sasa mama huyo analazimika kuendesha familia yake kwa biashaya ya kuuza ugoro na maziwa kidogo anayouza baada ya kamua Ngombe wake wawili.


Anasema kuwa, mume wake alitoweka nyumbani miaka tisa iliyopita na kwenda kusikojulikana .
“Mimi na mke mwenzangu tuko kwenye bola la mume wetu lakini hatujui alipo, yeye aliondoka tu hatuji alienda wapi,” anasema mama huyo.

Mama huyu anasema kuwa, baada ya kuona maisha yanazidi kuwa magumu, aliamua kwenda nyumbani kwao kuomba Ng’ombe ambapo alipewa wawili anaowakamua kwa sasa.

Anasema kuwa, ana shamba eka moja lakini hawezi kulilima lote jambo linalofanya maisha yazidi kuwa magumu.

Mama huyu anasema kuwa, jambo la kusikitisha wakati mwingine hata akilima shamba hilo dogo, ndugu zake wanaweza kuingiza ngombe wakala mazao yote.

Anaeleza kuwa, sababu inayowasukuma kufanya hivyo ni hali ya watu wa jamii hiyo kuthamini zaidi mifugo kuliko jambo jingine lolote.

Naye Matha Okida anasema kuwa, kabla ya mume wake kufariki dunia aliwatelekeza yeye na wake wenzake jambo lililofanya aamue kuondoka katika Kijiji hicho na kwenda kutafuta maisha maeneo mengine.

“Nilivyoona masha yamekuwa magumu, nilirudi nyumbani kwetu nikawaambia mume mliyenipa amemaliza Ng’ombe wote, kwa hiyo nipeni Ng’ombe nikatunze watoto wangu ama mnitunze,” anasema Okida:

“Hawakunipa Ng’ombe wala kunitunza, nikaamua kuanza kuuza ugoro na nikaondoka nyimbani nikaenda Kijiji vha Endonyongijape kata ya Kitwai nikawa napika makande na kuwauzia wawindaji, nikipata fedha naenda kuwapekeea unga watoto wangu.”

Anasema kuwa, sababu kubwa ya kutelekezwa kwa wanawake ni baada ya waume zao kumaliza Ng’ombe wote kwa kuwauza huku fedha zikiishia kwenye ulevi.

“Wake tulikuwa wanne, lakini Ngo’mbe zilivyoisha alituacha wote kila mmoja akawa anaangaika kutunza watoto wake,”anasema mama huyo.

Wanawake hao wanasema kuwa, licha ya waume wao kuonekana kuwa na Ng’ombe wengi, wamekuwa wakiwauza na kula fedha zote na wanawake wa mjini wakirudi majumbani mwao wanakuwa wamemaliza fedha zote.

Hali hii pia inatajwa kuwa moja ya sababu ya kueneza Virusi vya ukwimi katika vijji vingi kwenye eneo hili, jambo lililofanya kuacha wanawake wengi wakiwa wajane huku wakiwa na mzigo wa kuendesha familia kubwa ambazo huachiwa.

Diwani wa kata ya Langai Jackson Lesikari na yule ya Orkasumenti Naftali Samuel wanasema kuwa, katika maeneo yao hakuna kabisa vitendo vya wanawake na watoto kutelekezwa.

Lakini Mtendaji kata ya Endonyongijape Mary Chisoji, anasema kuwa katika eneo lake wanawake wengi wameachiwa familia huku wanaume wakiwa wametoweka nyumbani ama wapo lakini hawatoi mchango wowote wa kuendesha familia.

“Mara nyingi mama akifukuzwa mama akifukuzwa huwa haondoki na watoto kwa kuwa watoto ni mali ya baba, na kama ukiwa kiburi ukienda nao wanaweza hata kukutenga,” anasema Chosoji.

Ofisa Elimu Msingi katika Wilaya ya Simanjiro Jackson Mbise, anasema migogoro katika familia kwa kiasi kikubwa inaathari katika elimu kwani, familia zikiwa na matatizo hata uudhuriaji wa watoto shuleni unakuwa wa tabu.

Naye Kaimu Mrugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Patrick Saduka, anasema utelekezwaji wa watoto katika jamii ya kifugaji siyo mkubwa sana.

Kauli hii haipishani sana na ile ya Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Simanjiro Kaanael Kaaya, anayesema kwa kiasi kikubwa vitendo hivyo haviripotiwi katika ofisi yake.

“Wengi wa watu Simanjiro ni Wamasai, kwa hiyo hata baba akitelekeza familia utakuta kuna watu wengine wanamsaidia mama, lakini hali ni mbaya kwenye miji mikubwa kama Mererani kwa sababu ya mwingiliano wa wati ila siyo masaini,” anasema Kaaya.

Sababu nyingine inayotajwa kusababisha utekelezwaji wa wanawake katika jamii ya masaini ni ndoa za mitara, ambapo asilimia kubwa ya watu wapo katika ndoa hizo.

Pia baadhi ya watu wakiingia kwenye dini kama za ukirsto, wanaacha baadhi ya wake zao kwa kisingizio kuwa, wakristo hawaruhusiwi kuwa na mke zaidi ya mmoja.

No comments:

Post a Comment