Monday, September 12, 2011

watanzania wanaanza ngono mapema sana.

Fredy Azzah

IMEBAINIKA  kwamba Watanzana wanaanza kufanya ngono wakiwa na umri mdogo zaidi hali inayosababisha kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi pamoja na idadi ya watu kuongezeka.

Takwimu zilizotolewa jana jijini Dar es Salaam na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na Idadi ya Watu (UNFPA), katika kongamano la Afya ya Uzazi kwa vijana, lililokutanisha makundi mbalimbali ya vijana, zilieleza kwamba wasichana ni  kundi lililoathirika zaidi.

Ofisa Mipango wa Ukimwi wa UNFPA Dk Chilanga Asmani, alisema takwimu za shirika hilo zinaonyesha kwamba asilimia 59 ya wasichana huanza ngono wakiwa na chini ya miaka 18 huku ikiwa ni asilimia nne ya vijana wanaoanza ngono wakiwa chini ya umri huo.

Kwa mujibu wa Dk Asmani, asilimia 14 ya wasichana wanaanza ngono wakiwa na umri chini ya miaka 15 huku wavulana wanaoanza ngono kwa umri huo wakiwa ni asilimia nane.

Kwa upande wa kuoa na kuolewa, alisema asilimia 15 ya wasichana wanaolewa wakiwa na kati ya miaka 15 na 19 huku ikiwa ni asilimia tano ya wavulana wanaooa wakiwa na miaka 18 mpaka 19.

Alieleza pia kwamba, asilimia 60 ya wasichana wa Kitanzania wanazaa wakiwa na miaka 20.

Alisema kuwa matokeo ya hali hiyo, ni moja ya sababu zinazochangia Tanzania ambayo ni nchi ya 10 dunia kwa kuwa na vijana wengi, kuwa na maambukizi makubwa ya ukimwi kwa vijana.

Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kuwa, asilimia 60 ya vijana wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 15 na 24 wameambukizwa virusi vya Ukimwi.

Kwa mujibu wa Dk Asmani, hali hiyo inachangiwa zaidi na wasichana wengi kulazimishwa kufanya ngono, kukosa ujasiri wa kukataa, umasikini na pia wengi kutotumia uzazi wa mpango.

“Ni asilimia 27 pekee ya vijana wanatumia uzazi wa mpango, lakini pia katika kongamano hili tutajadili sababu nyingine zinazochangia hali hii na kisha kesho (leo) tutakapo kutana na viongozi tutawaeleza,” alisema Dk Asmani.

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Afya na Utafiti Afrika  (Amref) DK Festus Ilako, kuna changamoto kubwa katika ukuaji wa uchumi nchini na ongezeko la idadi ya watu.

Alisema hali hiyo inaakisiwa na ukweli kuwa, zaidi ya vijana milioni 20 wa Kitanzania wanategemea wazazi.

“Amref tupo tayari kuhakikisha Tanzania inaweza kushinda changamoto mbalimbali zilizopo,  ndiyo maana tuna miradi mingi karibu nchi nzima inayolenga kuangalia afya ua uzazi pamoja na maendeleo kwa ujumla,” alisema Dk Ilako.

Mwisho

No comments:

Post a Comment