Hatuyapendi maisha haya, jamii inatuonea!
NI wazi kuwa chini ya jua hakuna mtu au binadamu yeyote anayependa
kudhalilishwa, kila mtu angependa kufanya kazi halali ili awe na uhakika na
kipato chake.Hivyo basi, ukilitambua hilo utakuwa na sababu ya kutumia
jicho la tatu na kutafakari mambo mbalimbali yanayotokea katika jamii.Baadhi ya watu ambao pengine jamii imekuwa ikiwaangalia
kwa jicho ambalo nadiriki kusema siyo sahihi, ni wasichana pamoja na wanawake
ambao huuza miili yao katika maeneo mbalimbali nchini.Watu wengi wamekuwa wakiwatupiwa lawama kutokana na
shughuli hiyo wanayofanya, kila siku wakipewa
majina mbalimbali kama vile machangudoa, dada poa, malaya na mengine mengi.Wakati jamii ikilitazama hivyo kundi hili, kwa upande wao
nao wanailaumu jamii kuwa ndiyo
iliyowafikisha hapo walipo.Hivi karibuni katika
mazungumzo na baadhi ya wanawake hao wanaofanya
shughuli hiyo katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, wengi wao wanasema
kutelekezwa na familia zao ama waume zao, ndiyo sababu kubwa iliyowafikisha wengi
wao hapo walipo.
Winfrida Rafael (49), ni mmoja kati ya watu hao mwenye
umri mkubwa na pengine mkongwe katika biashara hiyo kutokana na kuifanya kwa
takribani miaka 15 sasa tangu alipotelekezwa na mume wake.
“Nilikuwa ninaishi Mwanza na mume wangu wakati huo alikuwa
anafanya kazi katika benki moja, baadaye alifukuzwa kazi, tukahamia Dar es
Salaam na mwaka 1997 ndiyo alinikimbia kabisa na kuniacha na mtoto mchanga yeye
akakimbilia Mtwara,” anaeleza mama huyo.
Anafafanua kuwa, kutokana na ugumu wa maisha ndipo
alipolazimika kuingia kwenye biashara hiyo ili aweze kujikimu kimaisha.
Tangu mama huyo aanze kufanya biashara hiyo, mwaka 2002
alijigundua pia kuwa na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) ambayo hata hivyo
anasema hajui aliambukizwa kwa njia gani.
“Siwezi kujua kama huu ugonjwa nimeambukizwa na wanaume
ama ni katika kuuguza ndugu zangu kwa sababu nimewauguza ndugu zangu wengi
mpaka wakafariki na wakati ule kulikuwa hakuna elimu sana ya kutosha kuhusu ugonjwa
huu kwa hiyo kujikinga ilikuwa ni vigumu,” anasema Winifrida.
Anaeleza pia kuwa, pamoja na kuwa na ugonjwa huo pamoja na
kansa ya mguu aliyoipata baada ya ajali aliyopata mwaka 2005, analazimika
kuendelea kufanya biashara hiyo ili aweze kupata walau chakula cha kuishi.
Ni kutokana na hali hiyo anasema kuwa, afya yake imekuwa
ikizorota kwa kasi ambapo CD4 zake zimekuwa zikishuka na kuwa
kati ya 200 na 300 badala ya kuwa 600 hadi 1,000 kama zinavyohitajika katika mwili.
Anasema kuwa ingawa anajua hali hiyo inasababishwa na
kufanya ngono ambazo wakati mwingine anafanya zisizo salama, hana njia nyingine
ya kuweza kumsaidia kuishi.
Naye Diamonte Mandanda (29), yeye anasema amejikuta
akiingia kwenye biashara hiyo miaka miwili iliyopita baada ya kutelekezwa na mwanaume
ambaye ni raia wa Italia aliyezaa naye.
Anasema tayari baba
yake na mama yake walishafariki na kuwa yeye alikuwa akiishi kwa mama yake
mkubwa ambaye hata hivyo baadaye walishindana na kuamua kusaka mahali pa kuishi
na kujitegemea.
Akiwa anaishipeke yake na
kujiendeleza na shughuli ndogondogo, anasema alimpata mwanaume huyo wa
Kiitaliano ambaye walipenda sana na baadaye kwenda kuishi nchini Kenya ambako
baadaye familia ya mwanaume huyo ilimkataa na hivyo kurudi nchini (Tanzania) na
mwanae.
Hata baada ya kurudi nchini, Diamonte anasema baba wa
mtoto amekuwa hataki kutoa matumizi yoyote kwa ajili ya kumsaidia mwanaye hali
anayosema inamlazimu kufanya shughuli hiyo ili kutafuta riziki yake na mtoto.
Anasema kuwa, licha ya kuushirikisha ubalozi wa nchi hiyo (Italia)
juu ya suala hilo, mpaka sasa wameshindwa kumsaidia na anaendelea kuishi maisha
ya taabu yeye na mwanaye.
“Jamani mimi nawaasa wasichana wenzangu tusiwe na tabia za
kuwapapatikia wanaume wa Kizungu, kuna wasichana wengi sana wameachiwa watoto
na tunawalea sisi wenyewe na kibaya zaidi huko mitaani watoto wetu
wananyanyapaliwa kweli,” anasema na kuongeza:
“Hata ukienda dukani kutaka kununua kitu wanakucheka wanakuambia
kamwambie Mzungu akununulie, mpaka najiuliza kwani watoto wetu siyo binadamu,
kwa nini watu watunyanyapae,” anahoji dada huyo kwa uchungu.
Anasema kuwa, kwa mtu atakayeweza kumsaidia akaachana na
biashara hiyo, atakuwa amemsaidia kwa kiasi kikubwa kwani anachokitamani katika
maisha yake ni mtoto wake huyo kupata haki zake za msingi kutoka kwa mzazi
mwenzie.
Kwa upande wake, Josephine Rutta (26), anasema kuwa wazazi
wake wapo kijijini Mkoani Kagera na kwa kiasi kikubwa wanamtegemea yeye na sasa
mtoto mdogo na mzazi mwenzake hamsaidii kwa chochote.
Baadhi ya watu wanaojishughulisha na kundi hili lililosahaulika
ni taasisi ya Dhahabu Arts.
Katibu Mkuu wa taasisi hiyo, Hussein Wamaywa anasema
taasisi yake imeliona tatizo hilo na imeamua kulifanyia kazi.
Anasema kuwa, ili kupunguza kasi ya maambukizi ya Ukimwi kwa
wasichana hao, wameamua kuwapa elimu ya jinsi ya kujikinga dhidi ya virusi vya Ukimwi pamoja na kuwapa njia
mbadala ya kuachana kabisa na biashara hiyo.
Anasema kuwa, shughuli hiyo inafanikishwa kwa ushirikiano
na Rapid Fund Envelope (RFE), ambao
wametoa fedha kwa ajili ya kuwapa wasichana hao mafunzo pamoja na mikopo ili
wafanye shughuli nyingine na kuachana na biashara hiyo.
“Kutokana na hali
hiyo, tumeona kuwa njia pekee ya kupambana na hali hii ni kutoa elimu juu ya
Ukimwi, kinga na maambukizi pamoja na elimu ya ujasiriamali lengo likiwa ni
kuhakikisha tunawatoa kabisa katika janga hili,” anasema Wamaywa.
Anasema kuwa, walengwa watatoka katika kata 90 za Dar es
Saalam ikiwa ni kata 30 kwa kila manispaa na kwamba zaidi ya wasichana na
wanawake 3,600 watafikiwa.
“Kwa wateja wao kwa sababu hatuwezi kuwafikia moja kwa
moja, tutatumia matangazo ya redio kufikisha ujumbe,” anasema Wamaywa.
Anasema kuwa, tayari wameshafanya mafunzo kwa wasichana
wanaofanya biashara hiyo katika wilaya zote tatu za jiji la Dar es Salaam,
Ilala, Kinondoni na Temeke.
“Sasa kazi tuliyowapa ni kutengeneza vikundi na kubuni
miradi ambayo sisi tutawafadhili, tunataka wawasaidie pia na wenzao kwa kuwapa
elimu juu ya maambukizi ya ukimwi na ile ya ujasiriamali,” anasema.
Mwisho
Machangudoa:hatuyapendi haya, jamii inatuonea www.faceboo.com

No comments:
Post a Comment