Thursday, May 24, 2012


Uozeshaji wanafunzi, watoto wachanga unavyoshamiri Simanjiro

mmoja wa wanafunzi aliyefanikiwa kuendelea na masomo ya sekondari baada ya wenzake watatua lofaulu nao kuolewa wote.


Fredy Azzah

“SISI ukiwa na mtoto wa kike tayari unahesabu utajiri, sasa ni mtu gani mjinga utakubali kufa na njaa umwache mtoto akamalize miaka saba shuleni,” anasema Elibariki Kisongo mkazi wa Kirun’gurun’gu.

Mzee huyu wa makamu ya miaka 70, anasema kuwa licha ya kuwa na wasichana 13 aliozaa na wake zake watano hakuna hata mmoja aliyesoma.

“We acha ujinga bwana, nikiwasomesha alafu watakuja kunisaidia nini,” anasema mzee huyo anayesema huwaoza watoto wake wakioneka wakubwa ingawa anashindwa kujua huwa wanakuwa na miaka mingapi.


Kwa upande wake Martha Okida (50),  mkazi wa Orkesument,  anasema ili mtoto wa kike asome katika jamii ya kimasai, mzazi wake anahitajika awe na akili ya ziada.

“Siku hizi baada ya kujua kuwa kumuolewa kwa mtoto wa shule ni vibaya, wanawapeleka kwa mume wakiwa na miaka sita mpaka nane,” anasema mama huyo.

Anasema kuwa, kuna matukio mawili ya watoto wenye miaka nane walikuwa wameozwa kwa wazee wenye zaidi ya miaka 65, ambao hata hivyo waliwahi kuokolewa na watu wa Sirika lisilokuwa la Kiserikali la Nafgem na kwenda kuwasomesha mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Anasema pia kuwa, kwa wale walio shuleni wakitaka kuolewa hupewa mimba ili wafukuzwe shuke ama wazazi wao kuwaambia wafanye vibaya shuleni.



“Mimi ili mtoto wangu asiole, ilibidi niende shuleni niongee na walimu waje kuwachukua, lakini nikamwambia mwalimu nyumbani nitamkana ili baba asinipige, baba alipokuja na kutaka kunilaani akaambiwa nilienda shuleni nikafukuzwa Mungu akasaidia watoto wangu wakasoma,” anasema mama huyo.

Kauli ya mama huyo inaungwa mkono na Elibariki Morani anayesema hali ya kuwaozesha watoto wadogo walio chini ya miaka 10, yameshika kasi katika eneo hilo.

“Hawa watoto siyo kuwa wanaenda moja kwa moja kwa mume, kwakuwa utakuta tayari mzee amechukua mahari, basi inabidi wampeleke mtoto akalelewe na mama wa kijana aliyetoa mahari, akiwa mkubwa aanze kuishi naye kama mke,” anasema kijana huyo.

Hata hivyo, suala linalozua mjadala hapa ambalo hata kauli za watoa taarifa hazikufafanua, ni jinsi ya kutambua kwamba mtoto amekuwa na anaweza kuishi na mume.

Wakati morani akisema ni mtoto kutoka mazima, Jacobo Lemburis anasema kuwa, wakinamama ambao wanawalea watoto hawa wakijiridhisha kuwa mtoto anaweza kulala na mwanaume bila kujali ana miaka mingapi, basi anaruhusiwa kufanya hivyo.

“Kwa hiyo huku kwetu wanaoachishwa masomo ili waolewe ni wachache kwa sababu wengi hawapati hata hiyo nafasi ya kuingia darasa la kwanza,” anasema Lemburisi.

Lemburis pamoja na Martha, wanasema kuwa, moja ya sababu inayochangia hali hii ni wazazi kuwa na tamaa ya kupata mahari.

“Wanajua kabisa kuwa ni kosa kuozesha watoto lakini wanatamaa ya mali,” anasema Lemburisi.

Hata hivyo kwa upande wake Martha, anasema kuwa, kwa kiasi kikubwa wanasiasa wamekuwa hawakemei ipasavyo vitendo hivyo kwa kuhofia, kupoteza nafasi walizo nazo.

Mrakibu wa Polisi Simanjiro (ASP) Felix Kikwale, anasema matukio haya yanaripotiwa kwa kiasi kidogo sana polisi kwani tangu mwaka huu uanze ni tukio moja tu limeripotiwa.

“Siyo kwamba haya matukio hayapo, tunajua ni mengi sana lakini watu hawaripoti polisi kwa kutojua sharia ama kwa tabia zao tu za usiri na kuogopa laana,” anasema Kikwale.

Mwenyekiti wa kijiji cha Lalumorijoi Jeremia Lemandi, anasema katika kata yake hivyo vitendo hivyo hakuna kabisa.

Pia Diwani wa kata ya Langai, Jackson Lesikari anasema kuwa, suala hilo lipo kwa kiasi kidogo ingawa anasema hana takwimu huku akisema suala hilo linasababishwa na watu kutokuwa na elimu.

“Wazazi wengi hawajui kuwa kumuozesha mtoto wa chini ya miaka 18 ni kosa, lakini kuna mashirika na serikali yamekuwa yakitoa elimu,” anasema Diwani huyo.

Naye Diwani wa Orkesument Naftal Samuel anaunga mkono kauli hiyo akisema kuwa, “Wananchi wangu wengi wameelimika, siyo rahisi ukute wakiozesha watoto.”

Mkuu wa Shule ya Sekondari Orkesument Jacobo Khahima   inayohudumia wanafunzi kutoka kata za Orukasument, Endonyongijape na Langai, anasema hana ushahidi wa kutosha juu ya suala hilo, ingawa kuna baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakiacha shule na wengine kupata ujauzito, jambo analosema linaweza kuhusishwa na hali hiyo.

“Hatuwezi kusema kuwa wanaolewa moja kwa moja, lakini wapo ambao wanaacha shule na wengine mimba, yote haya yanaweza kuambatana na suala la kuolewa,” anasema Mwalimu 

Anasema kuwa, tangu Januari mpaka sasa tayari wamepata wanafunzi wawili wajawazito mmoja aliyetakiwa kuwa kidato cha tatu sasa na mwingine wa kidato cha kwanza.

“Huyu wa kidato cha kwanza yeye alikuja na mimba kutoka huko kwenye shule yake ya msingi,” anasema Khahima.

Pia anasema kuwa, mpaka sasa wanafunzi sita wa kidato cha kwanza hawajaripoti shuleni hapo licha ya kupangiwa na Serikali na kuwa, mara nyingi watoto wengi wamekuwa wakienda likizo na kutorudi shuleni.

Joyce Michael mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo, anasema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakipewa mimba na matokeo yake kuacha shule.

“Wapo wengi tunaosoma nao wakiwa wameshaolewa, wakirudi likizo wanaenda kuishi kwa waume zao na wakipata mimba wanaacha shule, lakini mara nyingi hawa huwa hawaoni maana ya kusoma kwa sababu wanajua tayari wanawaume.” Anasema Michael.

Naye Naomi Meshilieki mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo anasema kuwa, katika kata ya Nangai anapotoka, suala la wanafunzi kuachishwa shule na kuolewa siyo jambo la ajabu.

“Tulipomaliza shule tulikuwa sita ambao tulifaulu, wenzangu wawili waliolewa na wengine waliacha shule wenyewe na sasa ni kama watatu tu tumeendelea,” anasema Meshilieki.

Mtendaji wa Kata ya Endonyongijabe Mary Chisoji anasema kuwa, suala la watoto kuachishwa shule katika kata yake ni kubwa.

Anasema tatizo hilo katika kata yake yenye shule moja tu ambayo ni  ya msingi ya Orkirungrung ni kubwa, jambo ambalo limechangia hata matokeo ya shule hiyo kuwa mabaya.

“Mwaka jana katika shule hii watoto wote walifeli, ilibidi tukutane wadau wa elimu kuangalia tatizo ni nini, moja ya yaliyogunduliwa ni wazazi kuwaeleza watoto wao wafanye vibaya ili waolewe ama wakachunge Ng’ombe,” anasema Chisoji.

“Hili tuliambiwa na badhi ya wanafunzi, na wamasai kwasababu wanaamini kuwa mzazi anaweza hata kukulaani ukikataa walichokwambia, nao kweli wakafanya vibaya, kwa hiyo hili suala la watoto wa kuachishwa shule lipo tena kwa sura nyingi tu.”

Kauli hiyo inaungwa mkono pia na Ofisa Elimu Msingi wa Wilaya hiyo Jackison Mbise, anayesema kuwa, kuachishwa shule huko huja kwa sura mbalimbali.

Anasema kuwa, moja ya njia hizo ni pamoja na wanafunzi kubeba mimba kwa makusudi ili wafukuzwe shule na nyingine ni utoro.

“Unaweza kukuta kati ya wanafunzi 194 wanaoanza shule, wanakuja kumaliza kati ya 40, 70 ama 100, wengine wanatoweka kwa njia kama hizi, wengi wa hawa wanaocha shule ni wasichana, ingawa na wanaume kwa uchache wapo na wao huenda kuchunga Ng’ombe”

Anasema kuwa, njia nyingine ni mzazi kuhama kabisa katika Kijiji kwa kisingizo cha kwenda kutafutia mifugo malisho, lakini ukweli ni kuwa wanaenda kuwaozesha watoto.

Katika Shule za sekondari hali ni mbaya zaidi katika eneo hilo la wanafunzi kuachishwa shule, hali inayofanya Ofisa Elimu Sekondari katika Wilaya hiyo Julius Mduma, kusema kila kukicha wanaumiza kichwa kuangalia jinsi ya kuangalia tatizo hilo.

Anasema kuwa, katika Wilaya hiyo yenye Shule za Sekondari 14, kati ya Wanafunzi 1976 wasichana wakiwa 934 na wavulana 1,042 waliopangwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu, walioripoti shuleni mpaka Aprili 16 mwaka huu walimuwa 1283 wasichana wakiwa 606 na wavulana 677.

“Kwa hiyo mpaka sasa Wanafunzi 491 wasichana kati yao wakiwa 272 na wavulana 219 hawajafika shuleni, Wilaya tumekuwa tukitoa gari kila mara likawatafute huko vijini bila mafanikio,” anasema Ofisa huyo.

Mbali na hao ambao walikwepa kuanza kidato cha kwanza, anasema pia hata wale ambao hufanikiwa kuanza kidato cha kwanza,   zaidi ya nusu huwa hawahitimu kidato cha nne.

Takwimu za Wilaya hiyo zinaonyesha kuwa, kati ya wanafunzi 157 walionza kidato cha kwanza mwaka 2004 wavulana wakiwa 70 na wasichana 87, waliohitimu kidato cha nne mwaka 2007 ni 47, wavulana wakiwa 30 na wasichana 17.

Pia mwaka 2005 walianza kidato cha kwanza wanafunzi 334, wavulana wakiwa 185 na wasichana 149, na waliohitimu kidato cha nne mwaka 2008 ni 154, wavulana wakiwa 94 na wasichana 60.

Mwaka 2006, wanafunzi 400 wavulana wakiwa 200 na wasichana 200 walianza kidato cha kwanza, waliohitimu mwaka 2009 walikuwa 350, wavulana wakiwa 195 na wasichana 155.

Mwaka 2007, wanafunzi 754 walianza kidato cha kwaza wavulana wakiwa 361 wasichana 393, walioitimu mwaka 2010 walikuwa 622 wavulana wakiwa 340 na wasichana 282.

Kwa mwaka 2008 Takwimu za Wilaya hiyo pia zinaonyesha kuwa, wanafunzi walioanza kidato cha kwanza waliwa 1,431 wavulana wakiwa 720 na wasichana 711, waliohitimu kidato cha nne mwaka 2011 walikuwa 763 wasichana wakiwa 363 na wasichana 363.

“Hilo ndiyo tatizo kubwa la  huku, na kwa kweli ukiangalia wasicha wengi wanaoacha shule tatizo ni mimba na kuolewa,” anasema Ofisa Huyo.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa Kushirikiana na Tamwa, umebaini kuwa sababu kubwa inayochangia mimba kwa wanafunzi kuwa nyingi katika eneo hili, ni Ngoma maarufu kama Esoto ambazo huchezwa usiku kucha na morani pamoja na wasichana ambapo wenyeji wanasema baada ya ngoma wanaume na wasichana hufanya ngono kwa kile kinachoitwa ni kuwafundisha wasichana hao ambao ni wachumba wao.

Mtendaji wa Kata ya Endonyongijape Mary Chisoji, anasema hilo ni jambo ambalo amewahi kulishuhudia na kuwa ni tatizo kubwa sana kata yake.

Anasema kuwa, baada ya kuchezwa ngoma hizo ambazo wasicha wanaoshiriki huwa wameshakeketwa na wapo tayari kwa kuolewa, hufanya ngono na Morani kwani tayari kimila wanatambulika kama ni wachumba na tayari huwa wamesha lipiwa mahari.

Morani Saitoti (38), mkazi wa Orkujit  anakiri kuwepo kwa ngoma hizo na kusenma kweli vitendo hivyo vinafanyika, lakini yeye anasema haoni tatizo kwani tayari wasicha ambao hucheza ngoma hizo ni wachumba wa watu.

“Sasa kuna ubaya gani kama utatoka na msichana wako ambaye umeshamtolea mali,” anahoji Saoitoti.

Pia katika eneo hilo, wasicha kuolewa wakiwa bado wakiwa ni wanafunzi ni tatizo kubwa.

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Simanjiro Steve Mibeyazo, anasema kuwa kesi za watoto kuachishwa shule zimekuwa zikifikishwa katika mahakama hiyo na maofisa watendaji wa kata  na zimekuwa zikitolewa uamuzi.

Hata hivyo anasema sheria iliyopo sasa ina changamoto kwa kuwa,  haisemi msichana aliyepata mimba anatakiwa achukuliwe hatua gani na kuwa,  amekuwa akitumia uzoefu wake katika kutoa adhabu kwa wote.

No comments:

Post a Comment