
Fidelis Butahe
KATIKA hali isiyo ya kawaida watoto wenye umri chini ya miaka 18 wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali au waliohukumiwa huwekwa sehemu moja na watu wazima katika Gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam jambo ambalo limesababishia baadhi yao kuingiliwa kinyume na maumbile na kuharibiwa vibaya.Tuhuma hizo nzito dhidi ya magereza zilibainika wakati Kamati ya Bunge ya masuala ya Ukimwi, ilipokuwa ikieleza mambo mbalimbali iliyoyakuta katika gereza hilo baada ya kufanya ziara, mbele ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Mambo ya Nje ulinzi na usalama inayoongozwa na Waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa.
Katika kikao hicho kilichofanyika ofisi ndogo za bunge jijini humo wiki iliyopita, walikuwepo maofisa mbalimbali wa Jeshi la Magereza akiwemo Kamishna Mkuu wa jeshi hilo, Augustino Nanyaro.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilizolifikia Mwananchi zinaeleza kuwa Kamati hiyo ya Ukimwi, ilieleza kwamba watoto chini ya miaka 18 wanaofika katika gereza hilo kwa makosa mbalimbali, utambulisho wao huonyesha kuwa wana miaka 19 hadi 20.
Taarifa hizo zilifafanua kwamba watoto hao ambao hukaa na wakubwa muda wa mchana na usiku huhamishiwa sehemu nyingine na kuingiliwa kinyume na maumbile kutokana na mazingira yalivyo ya kukosa pa kukimbilia.
“Waligundua mengi sana, walisema kuwa watoto hao wengi wameharibika sehemu zao za siri. Kutokana na hali hiyo wanaowafanyia vitendo hivyo huwatumia watoto hao kuingiza simu sigara, bangi na madawa ya kulevya gerezani. Wanaingiza vitu hivyo kwa kutumia sehemu zao za siri zilizoharibiwa,” kilisema chanzo cha habari kutoka kamati hiyo na kuongeza;
“Unajua huwa wameharibika kwa hiyo sehemu zao huwa wazi na kubwa kiasi kwamba ni rahisi kuficha simu, bangi, sigara na madawa ya kulevya bila kujulikana.”
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Rosweeter Kasikila alipotafutwa na gazeti hili jana alisema kuwa katika kikao hicho walipendekeza wakubwa kutengwa na watoto na kushauri upelelezi wa kesi kufanywa mapema ili kupunguza msongamano wa watuhumiwa.
“Hali sio nzuri yaani sehemu ya kuwekwa watu 40 wanawekwa watu 180…, jambo ambalo hatukulipenda ni jinsi watoto walivyokuwa wakiwekwa sehemu moja na watu wazima kwa sababu hujifunza mambo mengi ambayo si mazuri kwa umri wao” alisema Kasikila.
Alifafanua kwamba kitendo cha watoto kukaa sehemu moja na watu wazima ndio kinasababisha hata kufanyiwa vitendo vichafu ikiwa ni pamoja na kuingiliwa kinyume na maumbile.
“Tulieleza wazi kwamba watoto wanatakiwa kutengewa sehemu yao kwa sababu wakiwa wao wenyewe si rahisi kufanyiwa vitendo hivyo,” alisema Kasikila.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, katika kikao hicho maofisa wa magereza alipoulizwa kuhusu umri wa watoto hao walisema jambo hilo lipo ila hushindwa kufanya lolote kwa kuwa vielelezo vinavyoletwa huonyesha kuwa umri wao umezidi miaka 18.
Habari zaidi zilieleza kwamba maofisa hao walisema hali hiyo inatokana na mfumo uliopo na kwamba unatakiwa kufanyiwa kazi.
Chanzo kingine kilisema kamati hiyo iliamuru watoto hao kutengewa sehemu zao ili kuwaepusha na mambo mbalimbali.
Kauli ya Magereza
Naibu Kamishna wa Magereza, Fidelis Mboya alipoulizwa na Mwananchi kuhusu hali hiyo, licha ya kukiri alisema asingependa kueleza kwa undani mpaka apelekewe maswali kwa njia ya maandishi.
“Nitumie maswali kwa maandishi ili na mimi nijibu kwa maandishi, hili jambo ni ‘very sensitive’ (nyeti sana), lete maswali nitakujibu kwa maslahi ya taifa,” alisema Mboya.
Matukio ya utata wa umri
Suala la umri wa watuhumiwa na hata wafungwa limekuwa gumzo siku za hivi karibuni baada ya hivi karibuni mawakili wa muigizaji wa filamu Elizabeth Michael maarufu kama Lulu anayekabiliwa na kesi ya mauaji, kuwasilisha ombi lao Mahakama Kuu ili mahakama hiyo iamuru kesi ya msanii huyo isikilizwe katika mahakama za watoto wakidai kuwa mteja wao bado ni mtoto.
Uamuzi huo ulikuja baada ya awali kogonga mwamba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Lakini, tayari katika mkutano wa Bunge la mwezi Aprili 14 mwaka 2010, aliyekuwa mbunge wa viti maalum (CUF), Mgeni Jadi Kadika wakati akiuliza swali alisema serikali haioni kuwa kuna ulazima watoto kujengewa magereza yao au kuwekwa sehemu maalum.
Alisema hilo linatakiwa kufanyika kwa kuwa watoto hao wanapokuwa gerezani hukutana na wafungwa wenye tabia mbalimbali kama wizi, ubakaji, ujambazi na kwamba watoto hao wanaweza kuiga tabia hizo.
Akijibu swali hilo aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki alisema kwa mujibu wa Sheria zinazoratibu, kuongoza na kusimamia masuala ya mahabusu, wafungwa watoto wanapopelekwa magerezani wanapaswa kutenganishwa na wakubwa.
Kagasheki alinukuu Kanuni za Uendeshaji wa Jeshi la Magereza (The Prisons Standing Orders) ya mwaka 2003, kifungu namba 502, vifungu vidogo vya (ii) na (iii), wafungwa watoto wanapopelekwa magerezani wanatenganishwa na wafungwa wakubwa.
Ends
No comments:
Post a Comment