Hatuyapendi maisha haya, jamii inatuonea!
NI wazi kuwa chini ya jua hakuna mtu au binadamu yeyote anayependa
kudhalilishwa, kila mtu angependa kufanya kazi halali ili awe na uhakika na
kipato chake.Hivyo basi, ukilitambua hilo utakuwa na sababu ya kutumia
jicho la tatu na kutafakari mambo mbalimbali yanayotokea katika jamii.Baadhi ya watu ambao pengine jamii imekuwa ikiwaangalia
kwa jicho ambalo nadiriki kusema siyo sahihi, ni wasichana pamoja na wanawake
ambao huuza miili yao katika maeneo mbalimbali nchini.Watu wengi wamekuwa wakiwatupiwa lawama kutokana na
shughuli hiyo wanayofanya, kila siku wakipewa
majina mbalimbali kama vile machangudoa, dada poa, malaya na mengine mengi.Wakati jamii ikilitazama hivyo kundi hili, kwa upande wao
nao wanailaumu jamii kuwa ndiyo
iliyowafikisha hapo walipo.Hivi karibuni katika
mazungumzo na baadhi ya wanawake hao wanaofanya
shughuli hiyo katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, wengi wao wanasema
kutelekezwa na familia zao ama waume zao, ndiyo sababu kubwa iliyowafikisha wengi
wao hapo walipo.

