Mussa Juma, Arusha
KATA za Ngarenaro na Unga Ltd, katika Jiji la Arusha, zimetajwa kuongoza kwa wasichana wanaojifungua kutupa watoto wachanga mkoani Arusha.
Mratibu wa kijiji cha kulea watoto yatima na waliotelekezwa cha Samaritan Arusha, father Josephat Mmari , aliyasema hayo juzi, wakati akipokea msaada wa vifaa mbalimbali vilivyotolewa na Chama cha Kuweka na Kukopa cha Wanawake wa Nanenane Arusha.
Father Mmari alisema kijiji hicho, kimekuwa kikipokea watoto waliotupwa mara kwa mara kutoka katika Kata za Unga Ltd na Ngarenaro jambo ambalo aliomba akina mama hao kusaidia elimu kwa wasichana kuacha tabia hiyo.
“Hata wiki iliyopita tumepokea mtoto mmoja kutoka Unga Ltd ambaye ameokotwa ametupwa na kibaya zaidi watoto hawa wanaotupwa tunawakuta wamejeruhiwa na wazazi wao na kupata ulemavu kutokana na kuwekwa kwenye mifuko na kuumizwa,”alisema Mmari.
Mwenyekiti wa Nane nane Woman SACCOs, Happiness Makundi , akizungumza baada ya kukabidhi misaada ya vitu mbalimbali, yakiwamo madaftari, sukari, sabuni,unga na fedha taslimu alisema, wametoa msaada huo kutokana na faida waliyopata.
Makundi alisema katika faida ya zaidi ya Sh 10 milioni waliamua kutoa asilimia moja kusaidia watoto yatima wa vituo vya Mtakatifu Paulo, Bethrehem na Samaritan kutokana na kuguswa na matatizo ya watoto yatima na waliotelekezwa .
Mwanachama mwingine wa Saccos, hiyo yenye wanachama 157, Angela Bayo alisema watajitahidi kupitia makundi mbali mbali ya akina mama kutoa ushauri waache tabia ya kutupa watoto baada ya kujifungua kwani ni jambo baya na ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za nchi.
Habari kwa hisani ya gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment