Samson Chacha, Tarime
MKAZI wa kijiji cha Gwitiryo, kata ya Nyamaraga, Wilfrida Nyakaware (20), amelazwa katika zahanati ya Gwitiryo Sirari, akiwa ameoza mguu huku hali yake ikiwa mbaya kutokana na kipigo cha mumewe.
Taarifa zilizonaswa na gazeti hili juzi zilisema baada ya kutoa kipigo hicho, mume huyo alimfungia mkewe ndani kwa siku mbili bila matibabu na kumsababishia maumivu makali na mguu kuanza kuoza.
Akizungumza na waandishi wa habari katika zahanati hiyo alikolazwa tangu Julai 7, mwanamke huyo alisema ameambiwa na madaktari kuwa inabidi apelekwe Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.
Wilfrida alisema, “tukio hilo la kupigwa na kuumizwa hivi lilitokea Jumapili iliyopita (Julai 3) saa 2 usiku wakati mume wangu (Nyakaware) alipotoka matembezini.
“Nikiwa napika usiku, mume wangu aliniagiza nimpelekee taa ya chemli niliyokuwa naitumia kupika. Nilichelewa kumpelekea hapo ndipo alipodai kuwa nina kiburi na kuanza kunipiga kwa fimbo kwenye miguu yangu na mikono.
“Baada ya kunipiga na kuniumiza nilipoteza fahamu na aliniacha ndani nikiwa katika hali mbaya. Nina mtoto wangu wa kwanza mwenye umri wa miaka miwili, nilishindwa kumhudumia.
“Wazazi wangu walipata taarifa kuwa nimepigwa nipo ndani ya nyumba naozea ndani bila msaada ndipo baba yangu Sabaya na mama Maria walifika na kunichukua hadi hapa hospitali nilipolazwa.”
Mganga wa zahanati hiyo, Dk. Stephen Mtimba, alisema kabla ya kumhamishia Bugando, wamempa huduma ya kwanza Wilfrida kwa kuosha mguu, ili kuondoa usaha kwenye vidonda vya mguu.
“Hata hivyo, hivi sasa tumeamua kumhamishia Bugando kwani hali ya vidonda hivi si nzuri, vinahitaji matibabu zaidi ya kujaza nyama zingine na kuondoa zilizooza vinginevyo mguu huenda ukakatwa kwa kuchelewa kufanyiwa ukwanguaji wa nyama zilizooza,” alisema.
Polisi wilayani hapa wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa Nyakaware amekamatwa na anahojiwa katika kituo cha Polisi cha Sirari.
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Tarime/Rorya, Joachim Massega, alisema mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.
IMEANDIKWA NA GAZETI LA HABARI LEO
No comments:
Post a Comment