Fredy Azzah
MIONGONI mwa makundi ya kijamii yaliyo na mahitaji maalumu, watu wenye ulemavu ni kundi linalokumbwa na adha nyingi zaidi katika jamii.Adha na mateso zinazoikabili jamii hii ni pamoja na unyanyasaji, ubaguzi hata wakati mwingine kuuwawa kutokana na sababu mbalimbali.
Mayasa Mikidadi (44), mkazi wa kijiji cha Kiluvya kilichopo katika kata ya Kiluvya wilayani Kisarawe ni mmoja walio katika jamii hii.Hata hivyo kama wasemavyo wahenga kuwa, "Hujafa, Hujaumbika, Mayasa alipata ulemavu ukubwani.Anasema kuwa hali hiyo ya ulemavu pia imemwinginza katika mateso ambayo sasa yanamfanya asitamani tena kuishi.
Mayasa anasema kuwa kama siyo hali ya ulemavu uliomjia ukubwani, elimu aliyonayo ya kidato cha nne, ingemwezesha kuishi maisha apendayo bila tatizo lolote.
Anasema kuwa alihitimu kidato cha nne mwaka 1984 katika Shule ya Sekondari Usagara iliyopo mkoani Tanga na kuchaguliwa kujiunga na chuo cha Kilimo mkoani Mtwara mwaka 1985.
Akieleza chanzo cha ulemavu wake, Mayasa anasema kwamba mwaka mmoja baada ya kuingia Chuo cha Kilimo Mtwara alipatwa na ugonjwa aliosema wa ajabu ambapo miguu yote ilikufa ganzi.
“Baada ya mwaka mmoja niliumwa ugonjwa wa ajabu miguu ilikufa ganzi," anasimulia.Anaongeza:"Nilizunguka hospitali zote za Tanzania, mwisho nikaishia kuwa mlemavu wa miguu, siwezi tena kutembea mwenyewe mpaka nisaidiwe. Nikakubali hali hii, naikubali.”
Anasema kuwa baada ya kuona ulemavu alioanao unamfanya ashindwe kuendelea na masomo mkoani Mtwara, alijiunga na Chuo cha Ufundi Masiwani, Tanga ambapo alisomea ushonaji ili aweze kujiajiri mwenyewe ambapo baadaye mwaka 1996 alipata mchumba na kuolewa.
“Mwaka 1996 nilipata mchumba akanioa, Mungu alitubariki tukajaliwa kupata mtoto. Mume wangu hakuwa na kazi bali alinitegemea mimi kuanzia kula, kulala na mambo yote ya msingi,” anaeleza Mayasa.Anaeleza kwamba, baadaye walihamia jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea kutafuta maisha.
“Hapo tulibangaiza hadi mwaka 2004 tukanunua kiwanja maeneo ya Kiluvya na kujenga chumba kimoja ambapo tulihamia na ndipo ninapoishi kwa sasa,” anasema Mayasa.Kwa mujibu wa mama huyo, baada ya kuhamia katika eneo hilo, mume wake alianza tabia ya kutorudi nyumbani na alipofuatulia, alibaini kwamba alikuwa na mwanamke mwingine.
“Alianza kubadili tabia na kuuza vitu vya ndani, baada ya muda akaniambia amechoka kukaa na mlemavu akaamua kuuza nyumba. Nilienda kutafuta utetezi WILAC (Kituo cha Msaada wa Kisheria) wakaweka pingamizi,” anasema Mayasa.
Baada ya mume wake kushindwa kutekeleza azima yake ya kuuza nyumba, alitumia njia nyingine ya kwenda kukopa benki kisha kuiweka nyumba yao hiyo dhamana.
“Alishindwa kulipa ule mkopo, watu wa benki wakaja kupiga mnada nyumba nikiwemo ndani. Nilienda mahakamani nikaweka pingamizi, nilikuwa nikihangaika mwenyewe yeye wala hakusaidia chochote na tayari tulikuwa tuna watoto wawili ambao ni Latifa na Salehe,” anaeleza Mayasa.
Anaeleza kuwa, baada ya kuweka pingamizi hilo la mahakama, benki iliahirisha kupiga mnada nyumba hiyo na kuanza kumtafuta mumewe ambaye alikopa fedha ambazo hata hivyo Mayasa anasema hajui zilifanyiwa jambo gani.
Mayasa anasimulia kuwa baada ya kumalizika mikiki mikiki hiyo, mume wake alikuja na njia nyingine, safari hii alitaka kumfukuza ndani ya nyumba ili yeye aingie na kuishi na mke mwingine.
“Alikuja na mke na watoto wanne na gari, akatoa vitu vyangu ndani na kuingiza vya mke mwingine, nilikaa nje hadi nilipopata utetezi kwa majirani,” anasema Mayasa na kuongeza:
“Alinipiga akanitengua bega na kumvunja mkono mtoto (Latifa) na kuniandikia talaka hapohapo," anasimulia akiongeza:"Sitasahau tukio hilo maishani, kwa sasa maisha yangu yamejaa shida na mateso kutokan na ulemavu huu.”
Mama huyo wa watoto wawili anasimulia kuwa pamoja na vituko hivyo, lakini mumewe hakuishia hapo bali alienda kushitaki kuwa amemwekea sumu, hivyo yeye (Mayasa) alikamatwa na kupelewa mahakamani ambapo huku akinyimwa dhamana na kuambiwa kuwa atapelekwa Segerea.
“Nadhani alihonga, ndiyo maana nikanyimwa dhamana, nililia sana lakini badaye nikakubaliwa dhamana.”Mbali na matukio yote hayo, mama huyo anasema kuwa jambo kubwa linalomuumiza kichwa kwa sasa ni hatua ya mahakama kuamuru nyumba yake anayoshi na watoto wake iuzwe ili wagawane mali na mume wake huyo aliyemsaliti.
“Sasa ulemavu nilio nao siwezi kwenda mahali, ndugu wa kunisaidia sina,"Anasema,"nimemuandikia Waziri Mkuu anisaidie, akanijibu kupitia Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya amekuja na kuniambia amepewa agizo na Waziri Mkuu anisaidie, lakini bado naona kuwa mbele yangu kuna kiza kinene.”
Mayasa anaeleza kwamba, kutokana na ulemavu wake huo na mambo kadhaa aliyopitia kutokana na mgogoro huo, kwa sasa anaishi na kupata chakula kwa kusaidiwa na majirani.“Wasiponipa chakula, nalala njaa, nimeshazoea kulala njaa na wanangu,” anasema kwa uchungu mama huyo.
Mayasa anasema kwamba, mmoja wa watoto wake amefaulu na kupangiwa kujiunga na Sekondari ya Gogoni, lakini badala ya kufurahia suala hilo yeye alilia kwa sababu alijua kuwa hana uwezo wa kumsomesha.
“Huyu ndiye mkombozi wangu, uwezo darasani anao, lakini sina matumaini tena na siwezi kumsomesha mwanangu,” anaeleza Mayasa na kuongeza:
“Naomba Serikali inisaidie suala langu lishughulikiwe haraka, lakini pia mtoto wangu asaidiwe ili asome. "
Analalamika,"Nyumba yenyewe ina mgogoro, maji sina kwa karibu na siwezi kutembea kwenda kisimani, nilijaribu kufanya biashara ya kuku, lakini mume wangu alivunja banda na kuwauwa kuku wote."
"Nimemkosea nini Mungu mimi?” anahoji mama huyu akibubujikwa na machozi.Katibu Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali linalohudumia viziwi wasioona (DBWITEFO), Andrew Koti, anasema wameweza kumtembela mama huyo na kusikiliza matatizo yake.
“Mama huyu tumemtembelea mara kwa mara na kumsikiliza, leo ndiyo tumemuunganisha (Mwananchi), ili kilio chake kisikike kwa wengi zaidi aweze kupata msaada,” anasema Koti.

No comments:
Post a Comment