Thursday, August 11, 2011

Ajinyonga kutokana na kuchoshwa na vipigo vya mkewe


Anthony Mayunga-Serengeti

MKAZI mmoja katika mtaa wa NHC mjini Mugumu Samson Kitoshi (32) amekufa baada ya kujinyonga kwa kamba chumbani kwake kwa kile kilichodaiwa kuwa amechoka kupigwa na mkewe kila wakati.

Tukio hilo limevuta umati mkubwa wa watu linadaiwa kutokea Agosti saba saa tano asubuhi chumbani kwake alipofunga kamba juu ya dari na kuning'inia hadi alipokata roho.

Akisimulia mkasa huo mtoto wa marehemu Rehema Samson (10) anayesoma darasa la 3 shule ya msingi mapinduzi alisema kabla ya kutokea kwa tukio hilo mama yao alimpa Sh 1,000 anunue sukari na vitafunio, lakini asimpe baba yao chai.
 

"Mama aliaga kuwa anaenda hospitali DDH kuwa anaumwa, baba akabaki akasema hatakunywa chai hiyo na kutuambia kuwa hatutamwona tena anatuaga na tusiingie ndani humo,"alisema mtoto huyo.

Na hawakuweza kuingia ndani kwa kama walivyoambiwa na baba yao, lakini baadaye alimua kutaka kumwamsha akidhani amelala anywe chai ndipo akakuta ananing'inia amekwishakufa na kupiga kelele kuomba msaada.

"Baba alikuwa amevua shati akawa amening'inia chini kuna meza nikaweka stuli ili nifungue kamba sikuweza nikapiga yowe majirani wakafika na kudai ameishakufa,"alisema.

Kuhusu migogoro ya ndani alisema kumekuwa na ugomvi wa mara kwa mara hasa mama yao ambaye anauza wanzuki anaporudi amelewa humfanyia vurugu baba yao.

"Hivi karibuni baba alifikia hatua ya kumtaka mama aondoke amechoka na mateso anayomfanyia, lakini mama alikataa kuwa hawezi kutoka na kudai yeye ndiye atatoka,"alisema.

Naye ndugu wa marehemu aishie kijiji cha Morotonga jina tunalo alisema kuwa marehemu ambaye alikuwa akisaga kwenye mashine ya dereva wa halmashauri Casian Shayo alikuwa akilalamika kupigwa na mkewe mara kwa mara.

"Huyu ni ndugu yangu hata leo amefika kwangu na akanikosa na kurudi nadhani alitaka kuniambia kitu, baada ya muda napigiwa simu kuwa amekufa kwa kujinyonga, amechoshwa na kupigwa," alisema.

Na kuwa amewahi kupigwa hadi kuchomwa kisu na kuwa wamejitahidi kumsihi huyo mwanamke , lakini kila akitoka kilabuni hufikia kumcharaza na kumfanyia matendo mengi ya dharau ya kuchukuliwa na wanaume.

Kamanda wa polisi wilaya Paulo Mng'ong'o alijaribu kumtafuta mwanamke huyo kwa njia ya simu na mara baada ya kujitambulisha kuwa yeye ni OCD alikata simu.

Hata hivyo baada ya muda mama huyo alifika hadi chumbani na kumkuta mume wake aking'inia huku anapepesuka kwa ulevi aliuliza,"marehemu amekuwaje kwani jamani, "alitolewa na polisi huku akishangaa.

Hata hivyo akitoka chumbani alipokelewa na maneno makali kutoka kwa wanawake wenzake waliokuwa na hasira," ulitaka afe ujitawale sasa amekufa tanua, unadanganya ulikuwa hospitali mbona umelewa gongo muuaji wewe,"alisikika wakisema.

Kutokana na maneno hayo makali mwanamke huyo alikaa chini kisha akalala chali na hakuweza kunyanyuka kabisa hadi hatua ya mwisho aliwekwa kwenye gari moja na mumewe marehemu kuelekea hospitali akiwa amefunikwa kanga wakionekana kama wamekufa wote.

Naye Shayo alikiri kuwa marehemu alikuwa anasaga kwenye mashine yake na kuwa kwa muda wa siku mbili alikuwa hajafika kazini kabisa," jana na leo hakuonekana na si kawaida yake kumbe kulikuwa na kitu kinamsumbua, napigiwa simu tu kuwa kajinyonga,"alisema.

Mwenyekiti wa mtaa huo Elias Nyamraba alisema kuwa wanasubiri ndugu za marehemu huenda wakasafirisha mwili wa marehemu kwenda kwao katika kijiji cha Issenye. Hadi tunakwenda mitamboni mke wa marehemu alikuwa bado yuko hospitali ya Nyerere DDH.

No comments:

Post a Comment